MWANSOKO 1991 MTINDO WA KITAALUMA

Sura ya 2: Mtindo wa kitaaluma Utangulizi Uzoefu wa kusoma makala za kitaaluma na kuhudhuria semina mbalimbali umeonyesha kuwa pamoja na maudhui mazuri ya makala hizi kumekuwa na ukiukaji wa kutosha wa taratibu za kimtindo ambazo zina nafasi muhimu sana katika maandiko na majadiliano yoyote ya kitaaluma. Ingawa mwandishi amekuwa akitoa madokezo ya hapa na pale katika semina hizi kuhusu kanuni za kimtindo na makosa yatokanayo na ukiukaji wa taratibu hizi, hata hivyo suala hili bado linahitaji kuchukuliwa kwa uzito wake kamili hasa kutokana na kuongezeka kwa dhima ya Kiswahili baada ya lugha hii kufanywa lugha ya taifa. Matokeo ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa yamekuwa ni uimarishwaji zaidi wa lugha hii ikiwa ni pamoja na kuipenyeza katika matumizi ya kitaaluma. Masuala ya kitaaluma kwa kawaida hayawi ya nchi moja tu peke yake, bali huhusisha na kushirikisha mataifa mbalimbali. Hii ina maana kwamba tuandikapo makala au vitabu vyetu vya taaluma mbalimbali katika Ki...